Social Icons

Friday, January 20, 2012

THE ORIGINAL OF EVIL

JUMA LA MAOMBI KWA VIJANA WA TAASISI ZA ELIMU YA JUU

[THISDASO]

6-12 NOVEMBER 2011

MADA ZOTE TOKA KITABU CHA PAMBANO KUU

E.G.WHITE

Imekusanywa na kupangwa na Pr Y.Juma

Chaplain Mwanza

ASILI YA DHAMBI-UOVU

[THE ORIGIN OF EVIL]

E.G.White Pambano Kuu sura 29, Toleo la Kiingereza

Katika fikra za wengi asili ya dhambi na sababu ya uwepo wa dhambi ni vyanzo vikuu vya mashaka yao juu ya maswala ya elimu ya Uungu. Wanapoona matukio ya kazi za mwovu, yakiambatana na vilio na misiba ya kutisha wanabaki na maswali, haya yote yanawezaje kutukia na kuwepo chini ya Mungu mwenye nguvu zote, mamlaka yote, hekima yote, upendo wote na asiye na ukomo? Hapa ndipo penye siri kuu na za ajabu zisizo na maelezo ya majibu. [Here is a mystery of which they find no explanation]

Na katika hali hiyo ya utata, mazingira ya kikomo cha uelewa na wasiwasi na mashaka, wengi wamefungwa na upofu dhidi ya ukweli uliofunuliwa wazi na Neno la Mungu na umuhimu wa Wokovu. Wapo baadhi ya wale ambao katika harakati zao za kuuliza na kutafuta asili ya kuingia na uwepo wa dhambi, wameangukia kutafuta kile ambacho Mungu hajakifunua wazi na hatimaye huishia kwenye ugumu wa kupata suluhisho la magumu ya matatizo yanayowakabili na hali hii huwapelekea na kuwajengea haiba na tabia ya mashaka na malalamiko yanayowapelekea kufilisika na kuwapokonya hali ya kumhitaji Mungu na hatimaye kupata udhuru [excuse ]nyingi za kukataa maandiko matakatifu. Wengine hata hivyo hushindwa kabisa kupata utoshelevu wa kuelewa tatizo la asili ya uovu kwa kuingiziwa vigezo vya mafundisho ya kimapokeo na tafsiri zinazoficha na kupindisha mafundisho ya Biblia kuhusu tabia ya Mungu, Asili ya Serikali yake, na kanuni za kushughulika na dhambi.

Haiwezekani kueleza asili ya dhambi na kutoa sababu ya uwepo wa dhambi. Hata hivyo yatosha kuelewa juu ya yote asili na hatma ya tabia ya dhambi ili kufanya ukamilifu wa udhihirisho wa haki na upendo/ukarimu wa Mungu katika kushughulika kwake na uovu. Hakuna kitu kinachofundishwa zaidi ndani ya maandiko kuliko ukweli kwamba Mungu hakuhusika na uingiaji wa dhambi na wala hakuondoa nguvu ya Uungu wake kwa makusudi ili dhambi iingie na wala hapakuwa na upungufu wowote katika serikali yake ambao unaweza kusababisha uasi na machafuko. Dhambi ni mvamizi aliyeingilia bila kutakiwa, hakuna awezaye kueleza wala sababu iwezayo kutosheleza maelezo ya jinsi dhambi ilivyoingia. Uingiaji na uwepo wa dhambi ni siri kuu ambayo haijafunuliwa na maandiko, kuitetea kwa namna yoyote ya uingiaji wake ni kuikubali. Dhambi ni uhasama baina ya upendo na sheria ya Mungu, iliyo msingi wa Serikali yake.

Kabla dhambi haijaingia duniani, kulikuwa na amani na furaha kote ulimwenguni, kumpenda Mungu kulikuwa jambo kuu kabisa na upendo kati ya viumbe ulikuwa hausimuliki, Kristo, ambaye ni Mwana wa pekee alikuwa pamoja na Baba wa milele, katika asili, tabia na makusudi, Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa vilivyo mbinguni, ikiwa ni vitu vya enzi, usultani, enzi au mamlaka. Wakolosai 1:16

Sheria ya upendo ndiyo iliyokuwa msingi wa serikali ya Mungu. Furaha na raha ya viumbe vyote vilivyoumbwa ilitegemea jinsi walivyoafikiana na kanuni za haki. Mungu hupendezwa na huduma ya upendo na uchaji toka kwa viumbe wake ambao hububujisha ustadi wa maarifa ya uumbaji wa Mungu na shukrani yenye msingi wa tabia yake. Mungu hana furaha na alazimishi viumbe wamtii. Ametoa uhuru kamili wa dhamiri ili viumbe wote wamtumikie kwa hiari na siyo kwa shurti.

Lakini mmoja wa viumbe wake alichafua na kuvuruga mpangu huu wa uhuru. Dhambi ilianzia kwa huyu aliyechafua mpango wa uhuru wa Mungu, ambaye ndiye alikuwa wa pili kwa Kristo, Mwenye heshima kuu mbele za Mungu. Kabla ya kuanguka kwake Lusifa alikuwa Kerubi wa kwanza afunikwaye, mtakatifu, asiye na waa. Rejea Mafungu yafuatayo: Ezekieli 28:6-17, Isaya 14:13-14.

Heshima ya kufunika ambayo baba aliitoa kwa Yesu, Lusifa aliaanza kuitamani, heshima ya Mwana, yaani ya Kristo ilimuhusu yeye tu, wala si mwingine. Hali ya kutoridhika ilianza kuonekana katika umoja wa ajabu wa mbinguni , Lusifa alianza kujitukuza na kujiinua. Lilikuwa ni chukizo baya mno kufikiri. Baraza la mbinguni lilishughulika na kumsihi Lusifa juu ya mabadiliko ya kujiinua, mwenendo, na nia yake. Mwana wa Mungu alijihusisha kuvunja mwelekeo wa uasi wa Lusifa, alimweleza juu ya uzuri, haki na Utakatifu wa sheria ya Muumbaji. Onyo lilitolewa kwamba kama atajitenga na sheria yaani tabia ya Mungu, basi atakuwa amemdharau Muumbaji wake na kujiletea uharibifu mwenyewe, lakini onyo hili lilipingwa na Lucifa. Lucifa aliendelea kumwonea wivu Kristo, Kiburi kiliongeza tama ya ukuu wa lucifa, akawa mtaka makuu, heshima kuu aliyokuwa nayo ilimfanya aone kuwa yeye naye alipaswa awe katika utatu wa Uungu na hasa katika nafasi ya Kristo. Alikaza nia yake ya kufanana na Mungu Isaya 14:14, lakini mwana wa Mungu pekee ndiye aliyekuwa na cheo hicho, yaani Yeye ndiye aliyekuwa katika umoja na Baba, kwa kila mashauri Kristo alishiriki.

Hali ya kutoridhika kwa Lucifa ilipelekea uasi mkuu uliohusisha karibu theluthi ya malaika wa mbinguni walioungana naye dhidi ya serikali ya Mungu. Kundi hili asi la malaika lilishambulia tabia ya Mungu ambayo inatawala enzi yote. Lucifa na malaika hawa waasi pia walihoji uhuru na uhiari wa serikali ya Mungu, uasi huu uligharimu uvumilivu, ushauri na maonyo mengi toka kwa serikali ya Mungu, maonyo ambayo lucifa na malaika zake waliyapinga na kuyakataa kwamba si ya kweli, na akatumia uwezo wake wa udanganyifu kushutumu serikali ya mungu kwamba si ya haki.

Uasi wa lucifa na jeshi lake la malaika waasi lilipelekea kufukuzwa mbinguni, baada ya jitihada kubwa za maonyo na jitihada za kurudisha tabia ya Mungu ndani ya Lucifa. Anguko hilo ndilo mwanzo wa dhambi duniani, mwanzo wa madanganyo ya ibilisi na shetani, Ufunuo 12:7-9.

Roho ya uasi ya shetani bado inachochea hali ya uasi duniani kwa watu wenye hali ya kuasi. Shetani huwatangazia watu uhuru duniani, uhuru ulio kinyume na tabia na sheria ya Mungu. Shetani huwaaminisha watu kwamba wao ni wenye haki na kuwatafuta wengine waungane naye. Hudai kuwa wale wanaowaonyesha dhambi zao ndiyo wenye makosa, hufanya hivyo na kuondoa hali ya kujutia dhambi. Jinsi alivyosema mbinguni kuwa Mungu ni mkatili, ndivyo anavyowaingiza watu katika dhambi hata leo.

KUZA UFAHAMU:

Je maelezo yenye kukiri kuwa uwepo na uingiaji wa dhambi ni siri kuu[ mystery] ambayo mafunuo ya Biblia hayajaeleza uwazi wake kwa kina, na ilianzaje katika ukamilifu wa Mungu mwenyewe kwenye serikali yake ya mbinguni? Je maelezo haya yanakusaidiaje kumwelewa Mungu na kuiogopa dhambi?

Mwisho wa ukomo wako wa akili kufikiri juu ya uwepo na uingiaji wa dhambi unaweza kukusaidia kugundua kuwa mwisho wa akili yako kuna mwanzo wa Mungu? Kama kuelewa dhambi ni vigumu jaribu kutafuta urahisi wa Kifo cha Yesu aliye Mungu, na Mungu huwa hafi, lakini anakufa ili aiuwe dhambi!


UADUI KATI YA MWANADAMU NA SHETANI

[Enmity between man and satan]

E.G.White: Pambano kuu sura ya 30

Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino Mwanzo 3:15. Hii ni kauli ya Uungu iliyotangazwa dhidi ya shetani baada ya anguko la mwanadamu, pia ilikuwa ni utimilifu wa unabii uliotabiriwa katika vizazi vyote hadi mwisho wa wakati, ikiakisi utimilifu wa Pambano Kuu linalohusisha watu wa aina na mataifa yote watakaoishi duniani”

Tangazo la Mungu: “Nitaweka uadui” Huu uadui siyo kitu cha asili kilichowekwa au kilichokusudiwa. Wakati mwanadamu alipoasi Sheria ya Mungu, asili yake ya awali ikawa ovu, na akajumuishwa katika usawa wa uovu lakini tofauti na Shetani. Hapa uadui wa asili unatoweka kati ya mwanadamu muasi na mwanzilishi wa dhambi. Wote wanabaki kuwa waovu kupitia uasi. Kamwe shetani hapumziki mpaka apate kuelewa na kusaidiwa kwa kuwaingiza wengine kufuata mfano wake wa uasi. Kwa sababu hiyo malaika walioanguka dhambini na mwanadamu wangalikuwa katika kundi moja wameungana katika umoja wa kutokuwa na matumaini. Kama Mungu asingaliingilia kati Shetani na mwanadamu wangalikuwa katika kundi moja lililo kinyume cha mbingu; na badala ya uadui mkuu wote kumwegemea shetani, familia yote ya ubinadamu ingekuwa imeungana kwa uadui mkuu kinyume cha Mungu.

Shetani alimjaribu mwanadamu akaanguka dhambini, kama vile alivyosababisha malaika wakaasi, ili kwamba apate ushirikiano wa mapambano ya uasi wake dhidi Mungu. Kulikuwa na makubaliano kati ya Shetani mwenyewe na malaika walioanguka dhambini yenye chuki na vita dhidi ya Kristo; wakati huo huo upande wa pili kulikuwa kulikuwa na kutofautiana; Shetani aliposikia tamko kwamba kutakuwa na uadui kati yake na mwanamke na kati yake na uzao wa huyo mwanamke, alitambua kwamba juhudi zake za kuteka na kuharibu asili ya mwanadamu itakuwa imeingiliwa na kusambaratishwa na tamko hili na kwamba kwa namna fulani mwanadamu atakuwa amewezeshwa kupinga na kuzuia nguvu zake.

Uadui wa shetani dhidi ya uzao wa mwanadamu ulikuzwa na kuchochewa nguvu kwa sababu kupitia Kristo kumekuwa na tegemeo la rehema na upendo wa Mungu. Shetani alikusudia kuzuia mpango wa Mungu wa Ukombozi kwa mwanadamu na kutupilia mbali heshima ya Mungu kwa kuchafua taswira na sura ya Mungu na kazi ya uumbaji wake; alikusudia kuleta huzuni mbinguni na kuujaza ulimwengu vilio, misiba, na upweke. Shetani alikusudia kumnyooshea Mungu kidole kwamba uovu huu wote unaotokea sasa duniani ni matokeo ya kazi ya Mungu kwa kumuumba mwanadamu.

Kristo aliuweka uadui kati ya mwanadamu na shetani ili kumpinga Shetani. Bila kuwa na uwezo wa tamko hili la Neema ndani yake, mwanadamu daima angalikuwa mtumishi wa kutenda mapenzi ya Shetani, lakini kanuni hii mpya ndani ya mwanadamu ilianzisha mapambano na uwezo toka kwa Kristo ndani ya mwanadamu ili kupingana na utawala wa shetani. Kuichukia dhambi badala ya kuipenda huonyesha kanuni ya mbinguni.

Uhasama baina ya Kristo na shetani ulionekana dhahiri wakati wa kuzaliwa kwa Kristo mara ya kwanza duniani, ulimwengu haukuwa tayari kumpokea. Usafi, utakatifu na usahihi wa udhihirisho wa tabia ya Mungu ndani ya Kristo uliamsha chuki kubwa kati yake na watu wasiomcha Mungu. Hali ya Kristo ya kujikana nafsi ilikuwa ni shutuma kwa wenye majivuno, na wenye tamaa. Shetani pamoja na malaika waovu waliungana na watu wafedhuli kumpinga mwenye ukweli halisi.

NI NINI MATOKEO YA UADUI KATI YA MWANADAMU NA SHETANI KATIKA VIZAZI VYETU LEO?

1.Uadui ule ule uliodhihirishwa kwa Kristo na shetani, unadhihirishwa waziwazi leo pia kwa wafuasi wa Kristo. Shetani anawaletea wafuasi wa Kristo: [i] majaribu ili waanguke, [ii] shetani anawaletea chuki ili wapinge kanuni za kweli ya Mungu

[iii] Shetani anawaletea wakristo mateso ya kifikra , kimwili, kiroho na kijamii kupitia mawakala wake wa kibinadamu. 2Timotheo 3:12

2. Mawakala wa shetani daima wako kazini kuimarisha na kujenga mamlaka ya shetani na ufalme wake duniani ili kupinga serikali ya Mungu na kuwadanganya hata yamkini wafuasi wa kweli wa Kristo.

3. Shetani anatumia mawakala wake kuunda upya maandiko potofu na pia kupotosha maandiko sahihi ya Biblia ili kufikia goli lake.

4. Katika pambano la upotoshaji shetani ametumia na atatumia hata wajuzi na wataalamu wasomi wa dunia, na hatari zaidi hata wafuasi waliojitoa kikamilifu kwa Kristo, na jambo la kutisha zaidi, atatumia hata Wachungaji na watumishi wa injili waliojiingiza kwa siri. [GC 508]

5. Shetani anapambana kwa bidii kuwafumba macho wakristo ili wasitambue kuwa mapambano yao ni dhidi ya mamlaka za giza, Efeso 6:12-20, 1Petro 5:8

KUZA UFAHAMU- SHIRIKISHA WANA MAOMBI KUPATA UELEWA WAO:

Tamko la kuweka uadui kati ya Mwanadamu na Shetani, ni tamko la vita ya Ukombozi :

[i] Kristo kufanyika mwanadamu ili kuonyesha mwanadamu anaweza

kuishinda dhambi na Mungu anaweza kuonyesha upendo wa yeye kufa

ili kumponda shetani kichwa.

[ii] Ni tamko linalobainisha Pambano kuu alilonalo mwanadamu baina

ya wema na uovu. [Kristo na Shetani]

Je tamko hili la uadui lina kusaidia kumwona Mungu na wokovu wako? Au linaleta ugumu wa kuelewa mpango wa Wokovu?


MAWAKALA WA ROHO CHAFU [UOVU]

[AGENCY OF EVIL SPIRITS]

SURA 31

Uhusiano wa ulimwengu wa maumbile yanayoonekana na maumbile yasiyoonekana, na huduma za Malaika wa Mungu na ile ya mawakala wa roho chafu huelezwa dhahiri katika maandiko matakatifu na kujifungamanisha wazi katika historia ya mwanadamu. Malaika wema ambao huwahudumia warithi wa ufalme wa Mungu na kuwapa wokovu [Waebrania 1:14] hudhaniwa na baadhi ya wanadamu kuwa ni roho za wafu. Lakini maandiko hueleza wazi kuwa hawa siyo roho za wafu.

Kabla mtu hajaumbwa, malaika walikuwako, maana wakati wa kuweka misingi ya dunia malaika walikuwepo, wananukuliwa hivi “ Nyota za asubuhi ziliimba pamoja, na wana wa Mungu walipiga kelele za shangwe” Ayubu 38:7. Baada ya kuanguka kwa mwanadamu dhambini , malaika walitumwa ili kuulinda mti wa uzima ndani ya bustani ya Edeni kabla mtu hajafa. Kimsingi malaika wema kwa asili ni wakuu au bora zaidi ya wanadamu kima-jukumu na jinsi walivyoumbwa. Mtunga Zaburi anasema “ mwanadamu aliumbwa mdogo punde kuliko malaika” Zaburi 8:5.

Maandiko hutujulisha kuwa kuna idadi ya malaika wengi, nguvu na utukufu wa viumbe wa mbinguni wenye uhusiano na serikali ya Mungu na wenye uhusiano pia kazi ya ukombozi. Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni na ufalme wake unatawala juu ya yote. Nabii husema, “ Nilisikia sauti za malaika wengi waliokizunguka kiti cha enzi pande zote katika ukumbi wa Mfalme wa Wafalme wakisubiri “ malaika wenye enzi na ukuu” wamtumikie na kuleta furaha mbele kiti cha enzi, na sauti ikasikika ikisema Mhimidini Bwana enyi watumishi wake, ninyi mtendao neno lake Zaburi 103:19-21, Ufunuo 5:11. Kumi elfu mara kumi elfu na elfu kwa elfu ya malaika watumishi wa Mungu walikuwa ni watumishi aliowaona Daniel katika kiti cha enzi cha Mungu. Mtume Paul anasema juu ya malaika aliowaona “kama majeshi ya malaika elfu nyingi” Daniel 7:10. Waebrania 12:22. Malaika hawa huenda huku na huko kama watumishi wa Mungu, huruka kama umeme, mbio yao ni ya ajabu, Malaika aliyeonekana kwenye kaburi la Mwokozi, uso wake ulikuwa kama umeme, aliwafanya walinzi wazimie kama wafu. Wakati mfalme Senakeribu alimkufuru Mungu na kutisha wana wa Israel, Malaika wa Bwana akatoka na kuwapiga Waashuru katika matuo yao watu mia na themanini na tano elfu. Ezekiel 1:14, Mathayo 28:3-4; 2 Wafalme 19:35.

Malaika wa Mungu hutumwa kwa kazi nzuri juu ya watoto/ watu wa Mungu. Malaika huteuliwa kwa ajili ya wafuasi wa Kristo, hawa ni walinzi wa mbinguni, huweka ngao ya haki kuwalinda na nguvu za mwovu. Kwa Ibrahimu walileta ahadi ya mibaraka, huko Sodoma kumwokoa Lutu katika ajali; kwa Eliya malaika alitumwa wakati alipokuwa karibu na kuangamia Jangwani: kwa Elisha katika gari la Moto, kwa Daniel alipotupwa tunduni mwa Simba, kwa Petro alipofungwa na Herode ili auwawe, kwa Paul katika dhoruba kali baharini, kwa Kornelio ili apokee injili, na kwa Petro ili kupewa ujumbe wa Wokovu. Hivyo ndivyo Malaika wa Mungu wanavyowahudumia watu wa Mungu.

Kila Mfuasi wa Kristo hupelekewa malaika wa kumlinda, “ Malaika wa Bwana hufanya kituo akiwazunguka wamchao na kuwaokoa. Jambo hili shetani na mawakala wake malaika waovu hulitambua, na ndivyo walivyosema kwa kisa cha Ayubu “Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo-navyo?

MAWAKALA WA ROHO CHAFU NA UOVU

Roho wachafu, hapo mwanzo waliumbwa wakiwa malaika wema wasio na dhambi. Walikuwa wanalingana sawa na malaika wema ambao ni watumishi wa Mungu. Lakini wale walioanguka na kuasi sasa wanafanya kazi ya kupingana na Mungu na sheria yake, pamoja na kuwaharibu wanadamu. Waliungana na shetani katika kuasi kwake, na sasa wanafanya kazi pamoja naye kupigana na mamlaka ya Mungu. Historia ya Agano la kale hutaja kuwapo kwa malaika waovu, lakini pia wakati Yesu alipokuwa duniani roho hawa wachafu walijidhihirisha kwa hali ya juu kabisa. Soma kisa cha Marko 5:1-20, hapa pana kisa cha mtu aliyepagawa na mapepo yanayokadiriwa kuwa kati ya elfu tatu mpaka elfu tano. Kwa amri ya Yesu roho hawa wachafu walimtoka na kuwaingia Nguruwe na wengine baharini. Matukio mengine ya roh chafu yameandikwa katika Marko 7:26-30, Luka 4:33-36, Matendo 8:9-18, 13:8, 16:16-18.

Hakuna watu walio katika hatari kuu, ila wale wanaobisha kwamba hakuna mashetani na pepo wachafu ambao ni malaika wa shetani. Wengi hufuata mashauri yao huku wakidhani kuwa wanafuata mashauri ya nia zao wenyewe. Kadri tusogeleavyo mwisho wa wakati, ndivyo shetani anafanya juhudi kubwa kuwahadaa watu, kueneza habari mahali pote kwamba yeye hayupo na kuwanasa wengi katika upotofu wa mienendo yao.

Mdanganyifu huyu mkubwa pamoja na mawakala wa malaika zake waovu huogopa kwamba akijidhihirisha tutang’amua hila zake, kwa hiyo hajifunui moja kwa moja bali hutumia mawakala wake katika maumbile ya kibinadamu, na kuchochea burudani na maisha ya anasa yanayomwakilisha.

Usalama wetu upo kwa Kristo pekee na kukabidhi maisha yetu kwa uongozi wa Malaika wema wanaotuhudumia kila siku.

KUZA UFAHAMU

Je wajua roho chafu za malaika wa shetani hufanya kazi kwa bidii kupitia miujiza bandia inayofanywa na baadhi ya viongozi wa dini ndani ya madhehebu mbalimbali? Ufahamu huu utakusaidiaje kufahamu roho za uchafu hata katika taasisi yako ya elimu?


MITEGO YA SHETANI

[SNARES OF SATAN]

SURA YA 32

Pambano kuu baina ya Kristo na Shetani ambalo limekuwapo kwa takribani karibu miaka elfu sita sasa linaelekea ukingoni. Kwa hiyo shetani anajitahidi kufanya kazi maradufu ili kupingana na kazi ya upatanisho ya Kristo. Shetani anakusudia kuwashikilia watu katika giza la kiroho la kutokuamini mpaka kristo amalize kazi yake ya upatanisho dhidi ya wadhambi.

Hali ya kupoa na ubaridi itokeapo kanisani na duniani shetani hutulia maana hayo humpendeza na huitumia kam mtego wake kunasa wengi. Lakini watu wanapogutuka kuona hila za shetani na kuanza kuuliza maswali ya wokovu : Je tufanye nini ili tuokoke? Ndipo shetani huamka na kuingiza hali bandia ya wokovu wa kupotosha, ili kupinga kazi ya Kristo na ya Roho Mtakatifu.

Maandiko hufunua kuwa katika wakati fulani malaika walipohudhuria mbele za Bwana ili kuabudu, Shetani naye alihudhuria, siyo kwa nia ya kuabudu bali kwa nia ya kuendeleza udhalimu wake wa kupinga kweli na haki ya Mungu. Ayubu 1:6. Wakati Wakristo wanapokusanyika kwa ibada, naye uhudhuria ili kuyapotosha mawazo ya wenye kuabudu. Anapoona watumishi wa Mungu wanaandaa mahubiri, yeye naye huyanakili na kuyagushi, ili kuyapotosha kwa ujanja na ujumbe usiwafikie watu kama makusudi ya Mungu yanavyoelekeza na hasa kwa wale ambao tayari amewateka na mawazo yake ya upinzani.

Dalili mojawapo ya upotoshaji wa mawazo ni pale ambapo mtu angepaswa kuusikia ujumbe huo, humletea shughuli na mambo mengine ambayo yatamzuia asiusikie ujumbe huo. Shetani huwaona watumishi wa Mungu wakiwa na mzigo kwa ajili ya giza linalowafunga washiriki, huwasikia wakiomba Mungu awasaidie katika hali yao ya ulegevu. Kwa kutumia hulegevu huo shetani huwavuta wafuate mambo mengine labda ulafi, au ubinafsi, ili kuwapumbaza wasiweze kupambanua mambo ya lazima wanayohitaji.

Mdanganyifu mkuu anazo hila nyingi sana alizoziandaa ili kuwapotosha watu wa aina mbalimbali ambao atawapata. Ni nia yake kuingiza watu kanisani ambao siyo waongofu ili alete mashaka na hali ya kutoamini kwa Wakristo kwa ajili ya hao.Watu ambao hawana imani kwa Mungu huingia na kushika kanuni kanisani na kuhesabiwa kuwa ni Wakristo, kwa hiyo huingiza mambo ya kikafiri kanisani, na kuhesabiwa kuwa ni sehemu ya ukristo. Shetani anajua kuwa ukweli ukipokelewa kamili moyoni hutakasa maisha. Kwa hiyo hutafuta kuingiza mafundisho ya uongo yahesabike kuwa ni sehemu ya injili.

Tangu mwanzo watumishi wa Mungu walikuwa wakishindana na waalimu wa uongo siyo kuwa ni watu wabaya tu, bali ni waangamizaji halisi. Eliya, Yeremia, Paulo waliwapinga vikali watu ambao waligeuka wakaacha neno la Mungu na kufundisha mambo mengine, daima wapotoshaji waliokuwa wanahafifisha ukweli wa Biblia na imani ya kweli, hawakukubaliwa na watumishi wa Mungu waliokuwa watetea kweli.

Maelezo hafifu na potofu ya maandiko matakatifu na imani potofu katika makanisa ya ulimwengu ambayo huleta upinzani, mafarakano na tofauti katika makanisa ni matokeo ya kuacha ukweli wa maandiko Matakatifu, ili kuunga mkono nia zao, ili wapate udhibitisho wa nia zao, wengine husoma sehemu tu ya maandiko wakidhani kuwa inawaunga mkono ambavyo fungu zima la maandiko huwapinga. Maandiko hayo potofu hutumiwa kwa ujanja wa yule joka kuyatengeneza ili yaonekane kufaa kwa njia potofu na yadhaniwe kuwa yamo katika ukweli. Na wengine hutafsiri mifano na vielelezo kwa upande wao, wala hawajali ukweli wote wa maandiko. Hatimaye huleta tafsiri za makosa yao na kuieleza Biblia vibaya na kuyafanya kuwa ndiyo ukweli wa Biblia.

USALAMA WA KUNG’AMUA MITEGO YA SHETANI

Shetani anajua kuwa wote ambao hawajali maombi na kusoma Biblia hawawezi kuyashinda mashambulio yake. Kwa hiyo huvumbua kila aina ya vitu vyenye kuwashughulisha hata wakose nafasi ya kuomba na kusoma neno la Mungu.

Wakati Biblia inaposomwa bila maombi, bila kuwa na nia ya kujifunza, ukweli wake utapotoshwa na kudhani kuwa tafsri yako ni sahihi kumbe siyo sahihi.

Biblia nzima lazima isomeke kikamilifu bila kuhafifisha sehemu yoyote, neno la Mungu liko wazi kwa mtu yeyote anayelisoma kwa roho ya maombi na kujifunza.

Shetani ametupilia mbali Sheria ya Mungu katika makanisa mengi, na makanisa yamo katika utumwa wa dhambi, wakati makanisa hayo yakidhani kuwa yako huru.

Mungu amewajalia watu elimu nyingi ya sayansi, lakini hata wasomi na wataalamu maarufu wa elimu kama hawaongozwi na Biblia hupotea katika majaribio yao ya kuhusianisha sayansi na Biblia kimakosa. Elimu ya Kibinadamu ina sehemu tu na sehemu nyingine siyo kamili, kwa hiyo wengi hawezi kuhusianisha sayansi na neno la Mungu.

MAKOSA SABA AMBAYO SHETANI HUTUMIA KAMA MTEGO

Ishara za uongo, umizimu na ibada bandia.

Kukana Uungu wa Kristo.

Kukanusha kuwa shetani siyo kiumbe kamili ni kitu fikirika.

Kuja kwa Kristo mara ya pili ni tukio linalotukia mtu akifa

Dhana ya kuamini kuwa hakuna jawabu la kweli katika maombi.

Kutafsiri neno la Mungu kwa makusudi ya kukidhi matashi ya watu

Kuweka sayansi juu na kuikataa Biblia.


UONGO NA UDANGANYIFU MKUU WA KWANZA

[THE FIRST GREAT DECEPTION]

SURA 33

Katika historia ya mwanzo kabisa ya maisha ya mwanadamu, Shetani alianza harakati zake za kurubuni na kudanganya kizazi cha mwanadamu. Shetani aliyeanzisha uasi mbinguni alitamani kuwaunga pamoja naye wakazi wa dunia katika vita yake dhidi ya serikali ya Mungu. Adamu na Hawa walikuwa wakamilifu wenye furaha na watiifu kwa sheria ya Mungu. Utii wao ulikuwa ushuhuda wa daima na wa hakika kinyume cha madai ya shetani kwamba Sheria ya Mungu si ya haki na ni ya ukandamizaji. Hivyo kinyongo na wivu wa shetani dhidi ya makazi mazuri yaliyokuwa yametayarishwa kwa wanandoa hawa wasiojua dhambi yalikuwa ni kusudi lake kuyasambaratisha.

Shetani alikusudia kuwaangusha ili apate kuitawala dunia hii na kusimamisha utawala wenye kupingana na Mungu. Kama shetani angejifunua kama alivyo katika tabia yake angeweza kupingwa mara moja, kwa sababu Adamu na Hawa walikuwa wametahadharishwa mapema juu ya ulaghai wa shetani, hivyo alijitokeza katika njia za siri sana na za giza akiwa ameficha kusudi lake, ili kwamba atimize lengo lake. Hivyo akimtumia nyoka kama chombo chake, nyoka ambaye alikuwa kiumbe kizuri alimzungumzisha Hawa akisema, “ Ati hivi ndivyo alivyosema Mungu, msile matunda ya miti yote ya bustani? Hawa hakudhubutu kushauriana na adui akaanguka kwa ulaghai wake; mwanamke akamwambia nyoka; matunda ya miti ya Bustanini twaweza kula, lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema msiyale wala msiyaguse msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, hakika hamtakufa; kwa maana Mungu anajua ya kuwa siku mtakayokula matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu mkijua mema na mabaya” Mwanzo 3:1-5

Kama Hawa angeweza kukwepa na kukataa majadilianao na mjaribu, angeweza kuwa salama; lakini aliingia katika mtego huo na kuanguka katika jaribu la shetani. Hivyo ndivyo watu wengi leo hushindwa na mjaribu, wanatilia mashaka na kuhoji maagizo ya Mungu, na badala ya kutii kanuni za Mungu wanapokea na kufanyia kazi nadharia za kibinadamu ambazo ni mitego na nyenzo za shetani.

Adamu aligundua nini maana ya maneno ya mungu, “ Siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtakufa hakika! Adamu hakuona kuwa maana ya maneno ya Mungu ilikuwa hivyo alivyosema nyoka, Lakini Adamu pia akaanguka katika dhambi hiyo hiyo.

Mungu akasema kuwa adhabu ya kutotii maneno yake ni kurudi mavumbini, yaani kifo. “ Maana wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi” Mwanzo 3:19. Maneno ya shetani kuwa macho yenu yatafumbuliwa yalikuwa na ukweli kwa sehemu tu, maana macho yao yalifumbuliwa wakaona upumbavu wao. Wakajua mabaya na kuonja uchungu wa matunda ya uasi wao.

Mti wa uzima ulikuwa na uwezo wa kuendeleza Uzima. Adamu alikuwa na hiari ya kuuendea mti wa uzima bila kikomo na kuyafurahia matunda yake, naye angeishi milele. Lakini alifanya dhambi akazuiliwa asiyale tena matunda ya mti wa uzima, hivyo akawa mtu wa kufa. Hali ya kufa ilikuja kwa njia ya uasi, na mwanadamu asingekuwa na tumaini lolote la kuishi milele, kama Mungu kwa rehema zake asingemtoa mwanawe kuwa dhabihu kwa ajili dhambi za mwanadamu. “Mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wametenda dhambi” Kristo Yesu ndiye aliyebatilisha mauti na kufunua uzima na kutokuharibika kwa ile injili, ni kwa njia ya Yesu tu ndipo hali ya kutokufa hupatikana. “ Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele, asiyemwamini mwana hataona uzima” Warumi 5:12, Yohana 3:36.

UONGO, ULAGHAI, NA UDANGANYIFU MKUU LEO

Aliyewaahidi Adamu na Hawa uzima kwa kutotii sheria na Maagizo ya Mungu, alikuwa mwongo mkuu, na mdanganyaji mkuu. Akizungumza kwa njia ya nyoka huko Eden, alisema, “hamtakufa hakika” Hilo lilikuwa tangazo lake la kwanza kuhusu kutokufa kwa roho. Walakini tangazo hili ambalo ni uongo wa shetani ni mwangwi au udanganyifu uliopokelewa na sasa unahubiriwa na wahubiri wengi, na hupokelewa na watu maelfu, sawa kama vile udanganyifu huu ulivyopokelewa na wazazi wetu wa kwanza. Tangazo la Mungu ni hili “ Roho itendayo dhambi itakufa” [Eze. 18:20] lakini shetani akageuza kwa maana yake ya upotoshaji kuwa “Roho itendayo dhambi haitakufa

Ukweli wa wa matunda ya mti wa uzima ni kwamba, Kama mtu angeruhusiwa kutwaa matunda ya mti wa uzima baada ya kukosa na kuanguka dhambini, dhambi ingedumishwa milele, ndio maana mti wa uzima uliondolewa na hakuna hata mmoja wa wazao wa Adamu aliyeruhusiwa kula matunda ya uzima, kwa hiyo hakuna mwenye dhambi ambaye hudumu milele.

Baada ya anguko la mwanadamu, shetani aliwaagiza mawakala wake, malaika wa giza wawafundishe wanadamu waamini kuhusu umilele wa roho, kwamba hata kama mtu amekufa, roho yake huendelea kuishi milele. Baada ya kuwaaminisha watu namna hiyo huwaongoza waamini kwamba mtu mbaya afapo huendelea kuteseka katika uharibifu wa milele. Na kisha mdanganyifu huyu mkuu hutupa lawama na shutuma kwa Mungu kwamba Mungu si mwenye haki, huwaadhibu wote ambao hawampendezi na ya kwamba wakati wanapoteseka motoni namna hii, Mungu huwachungulia na kutosheka. Hivyo ndivyo shetani anatumia ulaghai kuchafua sura na tabia ya Mungu, Ukatili na hila ni wa shetani, Mungu ni upendo. Shetani ndiye huwashawishi watu kufanya dhambi na kuwaharibu ikiwezekana. Shetani hupindua mafundisho kuhusu upendo, rehema na haki ya Mungu ili yaonekane kuwa ni machukizo na ukatili wa kutesa watu katika moto huko ahera milele na milele.

UZUSHI NA MADANGANYO YA SHETANI

Mtu huwa afi, ila roho yake inakwenda peponi au kuzimuni.[Hamtakufa hakika]

[ Somo hili limekusudia kufundisha somo la hali ya wafu kama moja ya mada yenye

udanganyifu mwingi wa shetani]

Fundisho la Pargatori, moto wa milele kwa waovu na hoja ya Mungu kupendezwa kutazama watu wakiteseka.

Shetani huwafunga watu katika maisha machafu kwa mafundisho ya uongo ili wafe wakiwa ndani ya dhambi.

NUKUU YA TAFAKARI

Kama ingalikuwa ni kweli kwamba watu wote huenda mbinguni moja kwa moja wakati wanapokufa, basi sote tungalitamani kifo kuliko kuishi ili tuepukane na adha za dunia, na kuishi maisha yasiyo na adha mbinguni.


UMIZIMU

[SPIRITUALISM]

SURA 34

Mafundisho juu ya roho kutokufa yalitokana na udanganyifu wa kwanza wa shetani kwa Adamu na Hawa na upagani. Wakati wa kipindi cha historia ya Giza la Kiroho, mafundisho haya yaliingizwa katika imani ya kikristo na kuhesabiwa kuwa ni mojawapo ya kweli na yakageuza mahali pa maandiko yasemayo kuwa “ Waffu hawajui neno lolote” Mhubiri 9:5.

Imani ya kuwapo roho za wafu kuja kuwahudumia watu wanaoishi duniani, imeandaa njia ya kuingizia mambo potofu yaliyofumwa kwenye ukisasa wa kuongea na roho za wafu kimiujiza. Kama hao wafu wana ufahamu zaidi ya ule waliokuwa nao wakiwa hai, mbona sasa hawaji moja kwa moja na kwa uwazi ili kuwaelimisha wanadamu? Ikiwa roho za wafu huwazungukia jamaa zao walioko duniani, mbona hawakai na kuongea nao? Hapa ndipo shetani hufanya kazi ya umizimu kupitia malaika wake waovu ambao huonekana kama wajumbe katika ulimwengu wa roho.

Mkuu wa uovu yaani shetani, anao uwezo wa kuleta sura za watu waliokufa ambao ni jamaa zao, na kufanya maigizo ya watu hao kuonekana ni halisi kwa njia ya umizimu. Watu wengi hufarijika kuwa ndugu na rafiki zao wapo na wanaishi huko mbinguni. Bila kujihadhari na hatari yoyote, hutega masikio yao kwa “roho zidanganyazo , na mafundisho ya mashetani” 1Timotheo 4:1

Dhana hii ya Umizimu huwafanya watu wengi kufa bila kufanya matayarisho wakidhani wataombewa na kwenda mbinguni. Hivyo waliokufa bila kujitayarisha, yaani bila ya kujitoa kwa Kristo hudai kuwa wako katika furaha kuu huko mbinguni. Roho hizi za wafu zinazodai hukaa mbinguni, mara nyingine husema maneno ambayo huwa ni ya kweli na uongo kidogo sana, wakiisha kuaminiwa hutoa mafundisho yaliyo kinyume cha Biblia, na kwa kuwa mara nyingine husema maneno ambayo huwa yana kweli na kutabiri mambo ambayo hutokea, hivyo mafundisho yao ya uongo hukubaliwa kama mafundisho ya kweli ya Biblia. Hivyo ndivyo mizimu na roho za mashetani hufanya kazi. Roho hizi hukataa Uungu wa Kristo na kumhesabu mwumbaji kuwa na hali sawa na yao.

Wakati matokeo ya udanganyifu huo hukubaliwa kama ukweli, ndipo hutokea ishara ambazo ni kazi ya yule mwovu kuwadanganya watu wakaziamini kama ishara za Mungu. Watu wengi sana huamini katika hali ya kuongea na wafu au kuongea na mizimu na wanapokabiliwa na maonyesho ya wazi wazi ambayo hawawezi kuyakanusha, hukubali kuwa hayo hutoka kwa Mungu. Biblia inaonyesha umizimu wa Misri pale ambapo kwa msaada wa shetani wachawi wa Farao waliigiza kazi ya Mungu na kufanya miujiza, Kutoka 7:10-12. Mtume Paulo anashuhudia kuwa kuja kwa Kristo mara ya pili kutatanguliwa na “ kutenda kwake shetani, kwa uwezo wote, na ishara na maajabu ya uongo, na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea” 2Thesalonike 2:9-10. Yohana naye anasema, “Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu, naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya” Ufunuo 13:13-14

SHETANI HUTUMIA AKILI ZA WASOMI NA WATAALAMU KUINGIZA UMIZIMU WAKE NDANI YA WAKRISTO

Shetani hutumia wataalamu na wenye akili kuingiza na kuwaletea mizuka ya kiroho kwa njia ya akili sana yaani sura za rafiki na jamaa zao waliokufa, kana kwamba wanaweza kuongea nao, shetani hupendelea kuwapelekea mawazo ya ajabu na yenye misisimko ya kitaalamu yaliyojaa mambo ya upendo na fadhila tele. Huwafanya watu kupendelea mambo ya jinsi hiyo, na kupuuza mambo ya milele ya Mungu.

Kwa watu wenye kupenda anasa, wataka makuu, na wenye majivuno hali ya mizimu hufanya hila kwao kidogo tu. Kwa kuwa hali zao hufanana na zao. Shetani huona aina ya dhambi ambazo kila mtu huzipenda , halafu hutafuta nafasi ya kuzihimiza ili zifanywe. Huwajaribu watu na kuwatumbukiza katika hali ya kutokuwa na kiasi, ili apate kuwadhoofisha miili yao, akili na hali ya utambuzi ili wawe watu wasiofaa. Huwaaribu watu maelfu kwa njia ya

tamaa na kuharibu utu wao ili kukamilisha kazi yake .

Ili kukamilisha kazi yake, mizimu husema kuwa “ elimu halisi ni ile inayomweka mtu huru na sheria ya Mungu” Kwamba chochote ni haki, hata kama ni dhambi ya aina gani Mungu haihukumu, yaani hana lakusema juu yake, na kwamba dhambi zote hazina hatia” na kwamba watu wanapoamini dhamiri zao na matakwa yao ndiyo tosha kabisa, wala hawana haja ya sheria, na kuwa huo ndio uhuru, kwamba mtu ni juu yake kujiamuria yote.

Watu wanaopendelea kufanya dhambi hali wakijua, hushawishiwa na dhana hii hatari ya umzimu, na hujiweka wenyewe katika mikono ya shetani. Hujitenga na Mungu kwa hiari yao wenyewe, na malaika walinzi huwaacha peke yao bila ulinzi.

PAMBANO LA MWISHO LA UMIZIMU KWA WAKRISTO

Shetani huwafanya walimwengu waamini kuwa Biblia ni hadithi tu za kupiga chuku, sawa na zinginezo, huifanya Biblia ionekane kama kitabu tu kinachowafaa watoto wa jamii, lakini kwa sasa hakifai kutumika katika siku hizi zetu. Na mwokozi wa ulimwengu hufananishwa na mtu tu. Wale wanaoamini katika kuongea na roho hizi hawaoni muujiza wowote katika maisha ya mwokozi. Wanasema kuwa miujiza yao inazidi ile ya Kristo alipokuja hapa duniani.

Uzungumzaji wa wafu sasa umehesabiwa kuwa dini ya Kristo, na umevaa sura ya Kristo na mafundisho yake kukubaliwa waziwazi. Katika hali ya sasa sura hii ya umizimu ni ya hatari sana, ya kijanja sana, nay a hila sana, Wenye kuamini hali hii ya umizimu hukubaliana na mambo ya Kristo nusu na umizimu nusu, na hivyo Biblia hutafsriwa kwa namna ya kupotosha ili iwafurahishe wale wasioongoka.

No comments:

Post a Comment